03/07/2026
Sekta ya utalii na sanaa nchini inatarajiwa kupata msukumo mpya kupitia Tamasha la Sanaa na Kazi za Ufundi litakalofanyika mwezi Oktoba mwaka huu, likiwa na dhamira ya kuhamasisha uchumi wa ubunifu, kutangaza utamaduni wa Tanzania na kuwafungulia wasanii masoko ya ndani na kimataifa.
Tamasha hilo linaandaliwa na Tanzania International Tourism Festival (TITF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Sanaa za Ufundi Tanzania (TAFCA), likiwakutanisha wachongaji, wachoraji, wabunifu wa mavazi, watengenezaji wa vito, wafinyanzi na wasanii wengine wa kazi za mikono kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Hoteli ya Grand Melia Arusha, Mkurugenzi wa Tanzania International Tourism Festival, Ibrahim Jamal, amesema tamasha hilo limebeba maono ya kuiunganisha sekta ya sanaa na utalii ili kuongeza thamani ya kazi za ubunifu na kuwapa wasanii fursa za kibiashara.
Amesema mbali na maonesho ya sanaa, washiriki watapatiwa mafunzo kuhusu uongezaji thamani wa bidhaa, ulinzi wa haki za kazi za ubunifu, pamoja na mbinu za kufikia masoko ya ndani na nje ya Tanzania kupitia sekta ya utalii.