01/01/2022
2022 hii hapa sasa. Biashara gani nzuri ya kufanya mwaka huu wa 2022?
------------------------------------------------
Ukweli ni kwamba kila biashara ni nzuri na ina faida ndio maana unakuta biashara iliyomshinda mtu mmoja mwingine anaifanya na inamlipa.
Hivyo basi swala la kuwa biashara gani ni nzuri na yenye faida jibu lake ni kwamba biashara zote ni nzuri na zina faida.
JAMBO LA MSINGI NI HILI HAPA
Jambo la msingi ni kujua biashara gani ni nzuri kwako na biashara gani sio nzuri kwako. Hapa ndio panapotushinda wengi. Kuchagua biashara sahihi ni kazi ngumu sana.
Katika mambo mawili magumu kufanya maamuzi na kuchagua duniani la kwanza ni mpenzi sahihi na la pili ni biashara sahihi.
KUJUA K**A BIASHARA NI NZURI KWAKO
Unatakiwa kuangalia k**a hiyo biashara ipo kwenye orodha ya fursa zako. Kila mtu ana fursa zake. Ili fursa iwe yako lazima kuwe na mazingira wezeshi ya wewe kuiendesha biashara hiyo.
Mfano 1: Watu wawili wakiamua kulima. Wa kwanza akawa hana shamba, hana uzoefu, hana mtaji, hajui alime nini, na hajui soko lilipo. Mtu wa pili akawa ana shamba la urithi, amekulia kwenye mazingira ya kilimo alichokuwa anafanya baba yake, ana mtaji wa kulima, ana muda wa kutosha kusimamia shamba. Wa kwanza kilimo sio fursa yake. Wa pili ndio fursa yake.
Mfano 2: Mtu akiwa na gari la urithi akaamua kuligeuza gari hilo kuwa taxi na yeye akawa ndiyo dereva ukimlinganisha na yule mwenye gari la mkopo akampa dereva alete hesabu huku benki nao wakisubiri hesabu ya marejesho, yupi anaweza fanikiwa kwa haraka iwapo wote wana idadi sawa ya rasilimali nyenginezo?
TUNAZIJUAJE FURSA ZETU? HATUA TATU
HATUA YA KWANZA. Unatakiwa uanze kwa kuorodhesha rasilimali zote ulizonazo ikiwemo vitu, mali, fedha, maarifa, ujuzi, connection, muda, na kadhalika.
HATUA YA PILI. Ukimaliza kuorodhesha rasilimali ulizonazo orodhesha biashara zote unazoweza na ambazo unatamani kuzifanya.
HATUA YA TATU. Sasa linganisha rasilimali ulizonazo na biashara unazozitaka je ipi ambayo una rasilimali nyingi zaidi za kufanyia biashara hiyo? Utagundua kuna biashara unaweza kufanya kwa kutumia rasilimali ulizonazo. Anzia hapo na utafute vile ambavyo vinakosekana ili kufanya biashara hiyo.
HITIMISHO
Nakutakia kila la heri katika kuuanza mwaka wako vyema na kwa mafanikio. K**a umependezwa na makala hii basi usiache kutembelea https://www.miamia.co.tz/swahili mara kwa mara.