15/08/2014
SOLEMNITY OF THE ASSUMPTION OF MARY : KUPALIZWA KWA MAMA MARIA MBINGUNI - 15 AGOSTI 2014
“Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili” (Ufunuo wa Yohana 12:1)
Toka karne ya 4 Kanisa limekua likikumbuka “kulala” yaani Dormition, na baada ya kulala “kupalizwa” mbinguni (Assumption) kwa Mama Maria. Katika kuleta msisitizo wa umuhimu wake, Kanisa likasimamia zaidi katika “kupalizwa” kwake. Kwanini? Hii tutaona zaidi hapo baade. Leo hii na kila mwaka, tarehe 15 Agosti Kanisa linaadhimisha sikukuu hii ya “Imani ya Mitume” isiyopingika. Sio kwa uwezo wake mwenyewe, bali haswa kwa neema za Mungu, Kanisa linakiri kuwa Mama Maria alipalizwa mbinguni “mwili na roho”.
Kwa neema za Mungu, amefanywa Mtakatifu mkuu kuliko wengine wote. Mpaka itakapofika mwisho wa dunia hii (siku ya hukumu), Watakatifu wa Mungu walio mbinguni, humwona Mungu wakiwa katika hali ya roho tu (maana roho yaani “soul” kamwe haifi binadamu apatapo mauti. Mwili huoza, lakini roho hupokelewa na Mungu (k**a roho imetenda mema) ama hupokelewa na kuteswa na shetani kutokana na dhambi za mtu huyo na roho yake) . Hivyo Watakatifu wa mbinguni yawapasa kusubiri ufufuko wa miili yao siku ya mwisho ndipo wawe na ukamilifu wa binadamu (mwili kuungana tena na roho) ambayo ndiyo zawadi ya matendo yao mema. Hivi si k**a ilivyo kwa Mama Maria. Yeye yu mbinguni k**a binadamu kamili katika mwili na roho. Baada ya kumaliza kipindi chake mbinguni, yaani kifo chake (maana Mababa wa Kanisa na Wanateolojia wanaamini kuwa Mama Maria alikufa kifo cha kawaida cha binadamu ili kushiriki pia mateso ya Kristu kabla ya kushiriki utukufu wake baada ya kifo), hivyo punde baada ya “kulala” (Dormition), roho yake ikapokelewa na Kristu lakini pia mwili wake ukafufuliwa na kupalizwa na Kristu ili awe kamili katika ufalme wa mbingu. Hivyo Mama wa Mungu (Maria), pamoja na Kristu (Mungu Mwana) wanaishi katika hali zote mwili na roho mbinguni.
TUNAPATA WAPI FUNDISHO HILI LA IMANI?
Mapokeo ya Mitume (Apostolic Tradition) yanatufundisha imani hii lakini pia yakiambatanishwa na Biblia k**a kitabu kitakatifu. Rejea maandiko ya hapo juu yanayotolewa katika kitabu cha Ufunuo kilichoandikwa na Mtume Yohane kabla ya kifo chake. Mtume Yohane anapata ufunuo, anaona hekalu la Mungu lililoko mbinguni (Ufunuo wa Yohana 11:19), ndani mwa hekalu hilo analiona “sanduku la agano”. Kanisa na Watakatifu toka karne ya 2 wamemtafsiri Mama Maria k**a sanduku jipya la agano. Jinsi lile sanduku la zamani lilivokua safi bila doa, likibeba “mana” na amri kumi za Mungu (Waebrania 9:4) na jinsi Mungu alivyopenda kukaa humo pasafi (Kutoka 25:8) ndivyo hivyo hivyo Mungu alipoamua kuchagua sanduku jipya katika Maria ili aweze kukaa k**a “mana” ya kweli, kukaa k**a “amri mpya (Neno)” na mwisho kukaa k**a “Mungu” katika sanduku Maria. Mfano huo ni ukweli tosha kabisa ndio maana Injili ya Luka kwa makusudi kabisa inafanya mfanano kati ya sanduku la zamani na sanduku jipya (Luka 1: 39-45). Matokeo muhimu yaliyonakiriwa katika kitabu cha 2 Samweli 6:1-11 juu ya sanduku la agano la zamani ndiyo yanajitokeza tena kwa Maria. Kwanza sanduku linasafirishwa mpaka “mji mmoja wa Yudea” (2 Samweli 6:1-11), vivyo hivyo Maria baada ya kupata habari juu ya mimba ya Elizabeth, anasafiri mpaka “mji mmoja wa Yudea” (Luka 1:39). Mfalme Daudi katika kuliona sanduku la agano la zamani anacheza kwa furaha mbele ya sanduku hilo (2 Samweli 6:14). Vivyo hivyo mtoto Yohana Mbatizaji anaruka kwa furaha tumboni mwa mamaye Elizabeth baada ya kusikia sauti ya Maria (Luka 1:41). Tunaona pia mfanano wa sentensi zenye mshangao mkubwa wazitoazo Daudi na Elizabeth juu ya ugeni huo wa sanduku hizo mbili mpya na zamani. Daudi analipokea sanduku kwa kusema “....Litanijiaje (mimi) sanduku la Bwana? (2 Samweli 6:9), kwa upande wake Elizabeth anapomwona Maria anasema “Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?” (Luka 1:43). Mwisho kabisa tunaona kuwa idadi ya miezi ya ugeni wa sanduku hizo mbili huko Yudea ni sawa. Katika amri ya mfalme Daudi, Sanduku la kale likakaa nyumbani kwa Obed-edomu kwa miezi mitatu (2 Samweli 6:11). Tunaona pia kuwa Luka anatuambia Maria alikaa na Elizabeth kwa miezi mitatu pia (Luka 1:56)
Hivyo hatuna shaka kuwa Mama Maria ni sanduku jipya la agano. Haya yameandikwa na kusemwa pia na Mababa wa Kanisa, Watakatifu wa Mungu karne ya 2-4 za mwanzo (Mt. Hippolytus 170-236, Mt. Ephrem 306-373, Mt. Cyril 315-387, Mt. Athanasius 296-373, Mt. Gregory Thaumaturgus 213-270, Mt. Ambrose 339-397, Mt. Jerome 345-420 na wengine watakatifu wengi). Ndipo Kanisa na Watakatifu hawa wanavyosoma na kutafsiri maandiko katika kitabu cha ufunuo wa Yohana.
Kitabu cha ufunuo kinasema “Kisha Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa, na sanduku la agano lake likaonekana ndani ya hekalu lake. (ufunuo wa Yohana 11:19). Punde tu baada ya kusema hayo, Yohana anaongelea maono mapya juu ya mwanamke aliyevikwa taji la jua na kichwa chake kina nyota 12. Anasema ...” Na ishara kuu ilionekana mbinguni; mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi ulikuwa chini ya miguu yake, na juu ya kichwa chake taji ya nyota kumi na mbili (Ufunuo wa Yohana 12:1). Akiendelea kuelezea ufunuo huo, ni wazi kabisa Mama Maria (Sanduku jipya la agano) anaongelewa akiwa Malkia wa mbingu aliyefanywa na Mungu kuwa mkuu kuliko watakatifu wote kuliko hata malaika wote. Pia anaelezea jinsi Joka kubwa (shetani na malaika wake waovu) linavo jongea likipenda kumnyang’anya Mama mtoto anayekaribia kuzaliwa. Lakini mtoto huyu ndiye “atakayewachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Na mtoto wake akanyakuliwa hata kwa Mungu, na kwa kiti chake cha enzi (Ufunuo wa Yohana 12:5). Mtoto huyu ni Yesu Kristo, Mwana wa Maria.
SIKUKUU HII INA UMUHIMU GANI KWETU?
Katika kusheherekea sikukuu ya kupalizwa mbinguni Mama Maria, Kanisa linataka kutukumbusha vitu vikuu viwili:
1. Kwamba jinsi Mama Maria alivopalizwa mbinguni mwili na roho (assumption), ndivyo hivyo nasi tutakavyo palizwa siku ya mwisho. Roho zetu zinazopokelewa na Bwana siku ya mauti zitapata nafasi ya kukutana tena na miili yetu itakayofufuliwa. Nasi tutakua binadamu kamili nyumbani kwa Baba k**a ilivyo sasa kwa Maria. Hivyo sikukuu hii inatupa Tumaini kubwa mno kuwa Mungu ndiye muweza na hatatuacha miili yetu kuoza ardhini. Atatufufua siku ya mwisho
2. Pia Kanisa linatukumbusha umuhimu wa kumkimbilia Mama Maria katika maombezi yake kwetu. Maombezi yake ndiyo yenye matunda zaidi kuliko ya watakatifu wengine. Yeye huomba daima katika mapenzi ya Mungu. Hanyimwi lolote aombalo kwa Mwanaye. Tumkimbilie huyu Mama atulete karibu na Mungu tupate msamaha wa Mungu. Ndiyo maana katika historia ya Kanisa, Mama Maria amekua akiwatokea watu mbalimbali akiihasa dunia nzima kumfuata Kristu, kutubu na kutomkasirisha Mungu. Katika hali ya mwili na roho amewatokea watu huko Fatima, Lourdes Ufaransa, Guadalupe, Laus, Knock e.t.c
MAMA MARIA ULIYEPALIZWA MBINGUNI, UTUOMBEE SASA NA SAA YA KUFA KWETU